Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania na Uganda zaazimia kuzuia vifo vya mama na mtoto

Tanzania na Uganda zaazimia kuzuia vifo vya mama na mtoto

Nchi tisa duniani hii leo zimeazimia kuimarisha mifumo ya utoaji huduma za afya ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Nchi hizo ni Tanzania, Uganda, Bangladesh, Cote d’Ivoire, Ethiopia, Ghana, India, Malawi na Nigeria ambapo kwa usaidizi wa shirika la afya ulimwenguni, WHO na lile la kuhudumia watoto, UNICEF, zitaiongeza motisha kwa watoa huduma wa afya ili waweze kupanga na kuboresha huduma, sambamba na kuboresha ukusanyaji wa takwimu na upatikanaji wa vifaa vya tiba na maji safi na salama.

Mkurugenzi wa idara ya huduma za wajawazito na watoto watoto wachanga WHO Dkt. Anthony Costello amesema kila mama na mtoto ana haki ya kupatiwa huduma bora zaidi pindi wanapofika kusaka huduma hizo kwenye vituo vya afya.

Kwa kuboresha mtandao wa utoaji wa huduma ya afya kwa mama na mtoto, nchi hizo zinataka kutokomeza vifo vitokanavyo na magonjwa yanayoweza kuzuilika ifikapo mwaka 2030 kama ilivyoelezwa kwenye dira ya kimataifa ya mkakati wa afya ya kila mama kila mtoto na vijana barubaru.