Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuwajibike pamoja kusaidia wakimbizi- Guterres

Tuwajibike pamoja kusaidia wakimbizi- Guterres

Suala la jamii ya kimataifa kuwajibika pamoja katika kusaidia raia waliofurushwa makwao ni miongoni mwa masuala yaliyopatiwa kipaumbele wakati mazungumzo kati ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na Waziri Mkuu wa Uturuki Binali Yildirim mjini Istanbul hii leo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Istanbul, baada ya mazungumzo hayo ambayo Guterres ameelezea kuwa ni ya mafanikio makubwa wakati huu ambapo Uturuki inahifadhi idadi kubwa ya wakimbizi.

Katibu Mkuu ametaja aina ya kwanza ya kuwajibika kwa pamoja ni kusaidia wenyeji katika nchi ambako wakimbizi wameingia akisema usaidizi huo pamoja na miradi inayoweza kuchochea ajira, kuinua elimu, afya kwa wenyeji na wakimbizi.

Amesema aina ya pili ni wakimbizi kuhamia nchi ya tatu akisema idadi ya wanaochukuliwa iwe kubwa zaidi kuliko sasa akisema..

(Sauti ya Guterres)

“Mara nyingi tunasema kugawana mzigo lakini ningependa kusema kusaidiana uwajibikaji. Hii ni kwa sababu uhifadhi wa wakimbizi siyo tu wajibu wa nchi jirani na nchi zenye mizozo bali pia wajibu wa pamoja kwa jamii ya kimataifa.”

Guterres na Yildirim walizungumzia pia mizozo inayoendelea Afghanistan, Iraq na Syria ambapo Katibu Mkuu amezungumzia kile kinachopaswa kufanyika ili kushinda vita dhidi ya ugaidi..

(Sauti ya Guterres)

“Kamwe kama jamii ya kimataifa hatutaweza kushinda vita dhidi ya ugaidi iwapo hatutasaka suluhu ya kisiasa ambamo kwayo watu watapata faraja na watu wataona kwa dhati kuwa wanawakilishwa katika ngazi ya kisiasa.”