UNICEF yasaka dola milioni 42 kusaidia watoto Myanmar na DPRK

6 Februari 2017

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linasaka dola milioni 42 ili kusaidia watoto waliokumbwa na majanga huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Korea, DPRK na Myanmar.

Ombi hilo ni sehemu ya ombi kuu la dola bilioni 3.3 linalolenga watoto wote wenye mahitaji ya kibinadamu kwenye nchi 48 duniani kote.

Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Asia Mashariki na Pasifiki, Karin Hulshof amesema majanga asilia, mabadiliko ya tabianchi na mizozo inang’oa watoto kutoka maisha yao ya kawaida na kuwatumbukiza kwenye magonjwa na maisha duni.

Hivyo amesema fedha hizo zikipatikana, mathalani huko DPRK zitasaidai waathirika wa kimbunga Lionrock ambacho kiling'oa mazao, nyumba na hata kuharibu miundombinu ya maji.

Bwana Hulshof amesema huko Myanmar, fedha zitasaidia wakimbizi wa ndani hasa kwenye jimbo la Rakhine ambako watoto wanakabiliwa na uhaba wa lishe kutokana na ubaguzi na umaskini uliokithiri.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud