Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amri ya kuwazuia Waisilamu kuingia Marekani inakiuka haki za binadamu-UM

Amri ya kuwazuia Waisilamu kuingia Marekani inakiuka haki za binadamu-UM

Kundi la wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameonya leo kuwa, amri iliyotiwa saini na Rais wa Marekani Donald Trump mnamo Januari 27, ya kuzuia raia kutoka mataifa yenye Waislamu wengi kuingia nchini humo kwa siku 90,inakiuka wajibu wa haki za kimatiafa za binadamu katika taifa hilo.

Sheria hiyo imeyahusisha mataifa saba ambayo ni Iran, Iraq, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen.

Taarifa ya kundi hilo la wataalamu imesema kuwa hatua hiyo inakiuka kanuni za kutowalazimisha wakimbizi na wasaka hifadhi kurejea katika nchi wanazozikimbia, na ile ya kutobagua kwa misingi ya rangi, utaifa au dini.

Amri kama hiyo ni wazi kuwa ni ubaguzi kinyume na utaifa, inayosababisha kuongezeka kwa unyanyapaa dhidi ya jamii za kiisilamu, wamesema wataalamu hao ambao ni François Crépeau nayehusika na wahamiaji, Mutuma Ruteere wa haki za binadamu na ugaidi, Ben Emmerson anayehusika na utesaji, Nils Melzer na Ahmed Shaheed wa uhuru wa dini.

Wataalamu hao kadhalika wameonya kuwa sera hiyo ya Marekani inahatarisha watu kurejeshwa pasina ya tathimini sahihi binafsi na taratibu za usaka hifadhi ambapo watu hao wanatumbukia katika hatari ya kurejea katika maeneo wanayoweza kukabiliwa na utesaji na matendo mengine kinyume na binadamu.

Kadhalika wamesema kuwa amri hiyo inaathiri wenye uraia pacha ambapo wanasikitishwa kwamba watu hao wanaorejea Marekani watawekwa vizuizini kwa kipindi kisichojulikana, kisha kuondolewa kwa nguvu.