Shambulio la kigaidi lakatili maisha ya mlinda amani Mali

25 Januari 2017

Baraza la Usalama limeelaani vikali shambulio la kigaidi dhidi ya kambi ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, lililotokea kaskazini mwa Mali tarehe 23 mwezi huu na kukatili maisha ya mlinda amani mmoja kutoka Chad na kujeruhi wengine wengi.

Wajumbe wa baraza hilo wametoa rambirambi kwa wahanga, serikali ya Chad na MINUSMA, hususan kwa walinda amani wanao hatarisha maisha yao na kutoa wito kwa serikali ya mali kufanya uchunguzi wa kina na kuwawafikisha wahusika mbele ya mkondo wa sheria.

Vile vile wajumbe hao wamesema ugaidi ni tishio kubwa nchini humo na ulimwenguni kote na hivyo wamesisitiza haja ya mataifa yote kushirikiana kikamilifu na mamlaka zote kwa kuwawajibisha wahusika,wafadhili na wadhamini wa matendo hayo kwa mujibu wa majukumu yao chini ya sheria za kimataifa.

Baraza hilo pia limeeleza wasiwasi wake kuhusu kuzorota kwa hali ya usalama nchini Mali na ukiukwaji wa mpango wa kusitisha mapigano na kutoa wito kwa vyama nchini humo kutekeleza kikamilifu mkataba huo bila ya kuchelewa.

Kwa mantiki hiyo wajumbe hao wametoa ahadi ya kuunga mkono MINUSMA na majeshi ya Ufaransa katika juhudi zao za kuleta amani na utulivu wa kudumu nchini Mali.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter