Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamia ya maelfu ya wakazi wa Mosul wamo hatarini-OCHA

Mamia ya maelfu ya wakazi wa Mosul wamo hatarini-OCHA

Watu 750,000 wanaoishi magharibi mwa Mosul wanahofiwa kuzingirwa na mapigano yatakayoanza wiki zijazo na kuhatarisha maisha yao aidha kwa kulipuliwa au kutumiwa kama ngao, amesema Bi Lise Grande,  Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq.

Bi Grande amesema, siku mia baada ya operesheni ya Mosul kuanza, taarifa walizozipata kutoka eneo hilo ni za kutisha, kwani watoa misaada ya kibinadamu wanashindwa kufikia na hali inazorota kwa kasi zaidi kutokana na ukosefu wa mahitaji ya kimsingi, ambapo watu wengine wanapata mlo mmoja kwa siku na wengine wakikoka samani zao kujikinga na baridi..

(Sauti ya Lise Cut 1)

"Dawa muhimu, hususan dawa maalum, haijaweza kufika eneo hili la magharibi kwa muda mrefu sana, na kama wewe ni mtu mwenye ugonjwa wa kisukari ama ugonjwa wowote sugu, basi una taabu, una taabu kweli kweli."

Amesema wanafarijika kuwa watu 550,000 wameweza kusalia makwao mashariki mwa Mosul, na wanaatumai kuwa wadau watafanya kila wawezalo kuwalinda maelfu ya watu magharibi mwa Mosul kwani hatari ni kubwa zaidi na tunahofia usalama wao, akisema kile kinachotofautisha sehemu hizo mbili...

(Sauti ya Lise Cut 2)

"Kuna wasiwasi mkubwa kwamba kwa sababu jiographia ni tofauti na wilaya ni tofauti, hivyo mashambulizi yatakuwa tofauti na hilo linaweka raia wa magharibi katika hali ya hatari zaidi kuliko wale wa mashariki".

Amekumbusha kuwa ulimwengu umemakinika katika operesheni ya Mosul, lakini usisahau janga la kibinadamu baada ya hapo, kwani inatarajiwa kuwa milioni 3 hadi 4 ya wakazi wa Mosul, Hawiga na Tel Afar watasambaratishwa makwao kutokana na vita hivyo.

Kwa mantiki hiyo OCHA inajiandaa na mpangilio wowote utakaoletwa na mashambulizi, iwe ni msafara mkubwa wa watu wanaokimbia vita, uokoaji wa awamu ama mashambulizi yatakayo chukua muda mrefu.