Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya watoto wanaovuka kwenda Ulaya yaongezeka-UNICEF

Idadi ya watoto wanaovuka kwenda Ulaya yaongezeka-UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema watoto wapatao 25,800 waliwasili nchini Italia wakiwa peke yao kwa lengo la kusaka hifadhi barani Ulaya, kiwango ambacho ni ongezeko la zaidi ya maradufu ikilinganishwa na mwaka 2015.

Meneja mwandamizi wa masuala ya dharura UNICEF, Lucio Melandri amesema idadi kubwa yao wanatoka Eritrea, Misri, Gambia na Nigeria wengi wao wakiwa wavulana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 17.

Amesema watoto hao wako hatarini kukumbwa na ukatili, huku akitupia lawama mifumo ya sasa ya ulinzi wa watoto akisema inachukua muda mtoto mkimbizi kusajiliwa kuwa mkimbizi au mhamiaji.

Ili kukabili hali hiyo, UNICEF inatoa mapendekezo sita ikiwemo kuondoa utaratibu wa kuwaweka korokoroni watoto wanaosaka hifadhi, kuwapatia watoto huduma za elimu n afya bila kusahau kushughulikia vyanzo vinavyosababisha watoto kukimbia nchi zao na kusaka ukimbizi na uhamiaji.