Skip to main content

WHO kusambaza ARVs Benghazi

WHO kusambaza ARVs Benghazi

Shirika la afya duniani, WHO limesema kiwango cha maambukizi ya virusi vya Ukimwi huko Benghazi, nchini Libya kimeongezeka tangu kuanza kwa uhasama mwaka 2011.

Tathmini ya shirika hilo imeonyesha kuwa hali hiyo imesababishwa na kuporomoka kwa mfumo wa afya nchini humo ikiwemo mfumo wa upataji na usambazaji wa dawa.

Tayari Wizara ya Afya ya Libya imeomba WHO isaidia kupatikana na usambazaji wa dawa hizo kwani ukosefu wake unatishia uhai wa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.

Maandamano ya umma yameripotiwa kutaka hatua ya haraka kwa kuzingatia kuwa mwaka 2016 pekee watu 6330 nchini Libya walisajiliwa kuwa na VVU.