Skip to main content

Djinnit apongeza hatua ya CENCO huko DRC

Djinnit apongeza hatua ya CENCO huko DRC

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika, Saïd Djinnit amepongeza CENCO ambalo ni jumuiko la maaskofu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC , na pande husika kwa hitimisho la mazungumzo kuhusu mchakato wa kisiasa nchini humo.

Pande husika zilifikia makubaliano ya kisiasa mwishoni mwa mwaka kuhusu kufanyika kwa uchaguzi na taratibu za kipindi cha mpito kuelekea upigaji kura.

Bwana Djinnit ameshukuru viongozi wa CENCO kwa jitihada zao za kuendeleza mashauriano kulikowezesha pande husika kulegeza misimamo yao na hatimaye makubaliano ya kisiasa kwa maslahi ya amani na usalama nchini humo.

Amesihi pande kwenye makubaliano hayo kutekeleza kwa ukamilifu ili kutoa fursa ya kufanyika kwa chaguzi huru na za wazi na hivyo kuwepo kwa kipindi salama cha mpito wa kisiasa huko DRC.