Skip to main content

UM walaani vifo vya watoa misada na raia Mosul

UM walaani vifo vya watoa misada na raia Mosul

Huko mashariki mwa Mosul, nchini Iraq watu 11 wameuawa wakiwemo wafanyakazi wanne wa misaada na raia saba huku 40 wakijeruhiwa baada ya mashambulizi kutekelezwa katika matukio tofauti ikiwemo kwenye foleni ya kusubiri msaada.

Umoja wa Mataifa umelaani mauaji hayo ambapo mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq Bi Lise Grande,visa hivyo vimeripotiwa katika saa 48 zilizopita ambapo taarifa za awali zinasema kuwa watoa misaada na raia  hao wameuawa wakati wakiwa wamepanga mstari  kwa ajili ya misaada ya dharura.

Inadaiwa kombora lililipuka na kusababisha mauaji na majeraha kwa raia hao wasio na hatia ambapo Bi. Grande amesema  mashambulizi hayo hayakubaliki.

Amesema watu wanaosubiri misaada wako katika mazingira magumu tayari na wanahitaji msaada na lazima walindwe na sio kushambuliwa.

Amezikumbusha pande kinzani kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu na kulinda raia.