Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni Marekani zimeisha, mwelekeo ni yasemwayo baada ya uchaguzi

Kampeni Marekani zimeisha, mwelekeo ni yasemwayo baada ya uchaguzi

Umoja wa Mataifa umesema majigambo ya nyakati za kampeni za uchaguzi wa rais nchini Marekani yamepita na sasa ni wakati wa kuangazia kile kinachozungumzwa baada ya uchaguzi huo kufunga pazia.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema hayo wakati akijibu swali la wanahabari hii leo mjini New York, Marekani waliotaka maoni ya chombo hicho kufuatia kauli za Rais mteule Donald Trump wakati wa kampeni ya kwamba Umoja wa Mataifa ni taasisi isiyokuwa na maana yoyote.

(Sauti ya Dujarric)

“Kila wakati ambapo kuna mabadiliko ya uongozi kwenye nchi yoyote ile, hasa nchi ambayo ni mhisani mkubwa zaidi wa Umoja wa  Mataifa, huwa inatoa fursa ya fikra ya athari zitakuwa namna gani.Siwezi kuweka utabiri. Lakini kama nilivyosema uchaguzi umekwisha. Sasa kuna kipindi cha mpito. Tuna rais mteule na tuna matumaini tunaweza kuendelea kutarajia ushirikiano wa kina na uongozi wa Marekani ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa.”