Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ISIL na washirika wake wameendelea kupata pigo lakini tisho bado lipo:Feltman

ISIL na washirika wake wameendelea kupata pigo lakini tisho bado lipo:Feltman

Kundi la ISIL na washirika wake wameendelea kupata pigo la kijeshi , hali ambayo imedhoofisha uwezo wao wa kuhodhi maeneo, kukusanya rasilimali na kushikilia taasisi za serikali.

Hayo yamo kwenye ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliyowasilishwa kwenye baraza la usalama leo Alhamisi na msaidizi wa Katibu Mkuu wa masuala ya kisiasa Jeffrey Feltman .

Feltman amesema ripoti hiyo inatanabaisha tisho la amani na usalama wa kimataifa linalosababishwa na ISIL (Daeish ) na washirika wake. Ameongeza kuwa kufuatia kibano hicho hasa Iraq na Syria sasa kundi hilo linajitahidi kufidia hasara ya mapato yatokanayo na mafuta. Na kudhoofu kwa uwezo wa ISIL kumetoa fursa ya watu kuanza kurejea nyumbani

(SAUTI YA FELTMAN)

“Wakati operesheni dhidi ya ISIL nchini Iraq, jamhuri ya Syria na Libya zikizidi kupiga hatua, tunatarajia ongezeko la watu wanaorejea nyumbani katika maeneo yasiyo na mapigano. hata hivyo tisho la kimataifa la ISIL linaloongezeka, ni changamoto inayokuwa kwa amani na usalama wa kimataifa.”

Hata hivyo pamoja na hatua kubwa iliyopigwa ripoti imesisitiza kwamba tisho la ISIL lipo na linaendelea kupanua wigo. Miongoni mwa maeneo yaliyotajwa kkuathirika na ISIL ni Kusini Mashariki mwa Asia, Yemen na Afrika Mashariki.