Skip to main content

De Mistura ahimiza fursa ya misaada kabla ya mazungumzo ya Urusi na Marekani

De Mistura ahimiza fursa ya misaada kabla ya mazungumzo ya Urusi na Marekani

Juhudi kubwa zinafanywa na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Staffan de Mistura ili kusitisha uhasama na kuhimiza fursa ya misaada ya kibinadamu kabla ya mkutano wake na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey Lavrov na yule wa Marekani John Kerry mwishoni mwa wiki.

Huo ni ujumbe wa kutoka kwa Ramzy Ezzeldin Ramzy, naibu mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria alipozungumza mjini Geneva hii leo.

Wakati mataifa hayo mawili yakijiandaa kukutana, de Mistura anatia shime ya mjadala pia, kupunguza machafuko na jinsi ya kukomesha uhasama kabisa.

Ramzy Ezzeldin Ramzy, amesema hali ya madhila kwa wanaume, wanawake na watoto nchini Syria inazidi kuwa mbaya.

(SAUTI YA EZZELDIN RAMZY)

“Machafuko lazima yapunguzwe, ni lazima kukomeshwe mashambuzli ya makombora na mapigano, hususani yanayolenga maeneo ya raia , vituo vya afya, na maeneo yenye umati wa watu. Hii ni njia pekee Umoja wa Mataifa unaweza kutekeleza majukumu yake katika masuala ya kibinadamu.”

Kwa upande wa Aleppo Ramzy amesema pande zote Maghalibi inayodhibitiwa na serikali na Mashariki inayodhibitiwa na waasi zimetumbukia katika machafuko yanayoendelea, huku Mashariki kukifurutu ada na kukiwa na watu 250,000 waliokwama katika eneo hilo.