Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu la UM lakutana leo kumpitisha Guterres

Baraza Kuu la UM lakutana leo kumpitisha Guterres

Harakati za miezi Sita za kumsaka mrithi wa Katibu Mkuu wa sasa wa Umoja wa Mataifa zinafikia ukingoni leo ambapo Baraza Kuu la Umoja wa huo linatakutana asubuhi kupitisha tamko la Rais wa baraza hilo la kuridhia pendekezo la Baraza la Usalama la uteuzi wa Antonio Guterres wa Ureno kushika wadhifa huo.

Barua ya Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Peter Thomson kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa imesema kikao hicho kitaanza saa Nne asubuhi kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.

Bwana Thomson amesema kikao hicho kitakachoonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya mtandao ya Umoja wa Mataifa, UNWEBCAST,  kitakuwa cha wazi na kwa mujibu wa matarajio ya nchi wanachama, ni matumaini yake ya dhati kuwa waraka huo utapitishwa kwa kauli moja.

Waraka huo wenye aya Nne, unarejelea Ibara ya 97 ya Katiba ya Umoja wa Mataifa inayolipatia mamlaka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupiga kura au kupitisha kwa kauli moja jina pendekezwa kutoka Baraza la Usalama.

Halikdhalika waraka unapongeza mchakato mzima wa kupata Katibu Mkuu na hatimaye kueleza kuwa linamteua Antonio Guterres kuwa Katibu Mkuu wa tisa kwa awamu ya kuanzia Januari Mosi 2017 hadi Disemba 31 mwaka 2021.

Bwana Thomson amerejelea matukio ya awali ya uteuzi wa Katibu Mkuu akisema kuwa kama ilivyo kawaida, kupitishwa kwa waraka huo kutatoa fursa kwa wenyeviti wa makundi matano ya kikanda, sambamba na mwakilishi wa nchi mwenyeji ambayo ni Marekani, kuwasilisha taarifa zao.

image
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Peter Thomson. Picha: UN Photo/Cia Pak
Baadaye alasiri, Rais huyo wa Baraza Kuu ataitisha mkutano wa wazi usio rasmi ambamo kwamo Katibu Mkuu mteule, pamoja na wawakilishi wa nchi wanachama watazungumza.

Bwana Guterres ambaye aliongoza shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR tangu mwaka 2015 hadi 2015, alikuwa ni miongoni mwa wagombea 13 waliowania nafasi hiyo ya kuwa Katibu Mkuu wa Tisa wa Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu wa sasa Ban Ki-moon aliingia madarakani Januari Mosi 2007 na kuchaguliwa bila kupingwa kwa awamu ya pili tarehe 21 Juni 2011, anahitimisha jukumu lake Disemba 31 mwaka huu.