Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ethiopia yavutia mabilioni kutoka kwa wawekezaji katika viwanda:UNIDO

Ethiopia yavutia mabilioni kutoka kwa wawekezaji katika viwanda:UNIDO

Ethiopia imekuwa sumaku ya kunasa wawekezaji katika sekta ya viwanda nchini humo na kuvutia mabilioni ya dola katika miaka ya hivi karibuni.

Kauli hiyo imetolewa na LI Yong mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya viwanda UNIDO, katika kongamano kuhusu uwekezaji katika sekta ya kilimo na viwanda linalofanyika Addis Ababa, Ethiopia.

Bwana Yong amesema uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje katika taifa hilo la Pembe ya Afrika, umeingiza jumla ya dola bilioni 2 kwa mwaka 2015 pekee, na kuifanya Ethiopia kuwa lulu kwa wawekezaji hasa katika sekta ya nguo na mavazi.

Kongamano hilo la siku tatu, na la kwanza la kimataifa kuhusu uwekezaji katika sekta ya kilimo na viwanda limeandaliwa na UNIDO na serikali ya Ethiopia na linafanyika katika makao makuu ya tume ya uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afrika.