Walimu ni kichocheo cha SDGs, hivyo wathaminiwe- UM
Ikiwa leo ni siku ya walimu duniani, Umoja wa Mataifa umepigia chepuo suala la kuboresha maslahi ya walimu, mafunzo yao ili kuhakikisha hadhi yao inatambuliwa kwa kuzingatia kazi yao adhimu wanayotekeleza kila uchao. Amina Hassan na ripoti kamili.
(Taarifa ya Amina)
Wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la mpango wa maendeleo, UNDP, elimu sayansi na utamaduni, UNESCO, kuhudumia watoto, UNICEF na ajira ILO katika taarifa yao ya pamoja wamesema walimu wanasaidia watoto kujifunga na kuchanua katika stadi zao.
Kwa mantiki hiyo wana nafasi kubwa katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na hivyo lengo namba Nne haliwezi kufanikiwa iwapo walimu hawatapatiwa stadi za kutosha za kuwawezesha kufanya kazi yao.
Wamesema idadi ya walimu lazima iongezeke na hilo litawezekana iwapo watathaminiwa na kupatiwa mafunzo yanayokwenda na wakati na hivyo kwenda sambamba na maudhui ya mwaka huu ambayo ni Thamini Walimu, Boresha Hali zao.