Mauaji ya wasio na hatia Aleppo yakome hima: UNICEF

Mauaji ya wasio na hatia Aleppo yakome hima: UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF limetaka kukomeshwa hima kwa mauaji ya watoto mjini Aleppo Syria.

Katika taarifa yake UNICEF imesema juma hili pekee watoto zaidi ya 90 waliuwawa na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa katika shambulio ambalo shirika hilo limeliita lisilo na huruma.

Kwa mujibu wa UNICEF madaktari wamelazimika kuwaacha watoto wapoteze uhai wakati wanawahudumia wengine huku wakikabiliwa na upungufu wa madawa. Kadhalika maelfu ya watoto hunywa maji machafu kutokana na kushambuliwa kwa pampu za maji na nyingine kuzimwa.

Kama vile haitoshi watoa misaada ya kibinadamu wameuwawa, magari ya misaada yameharibiwa na makombora huku dunia inatazama matukio haya ya kutisha, imesema taarifa ya UNICEF na kusisitiza kuwa mauaji ya wasio na hatia lazima yakomeshwe.