Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake wanaathirika zaidi na vikundi vyenye msimamo mkali:UNAMA

Wanawake wanaathirika zaidi na vikundi vyenye msimamo mkali:UNAMA

Naibu mwakilishi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa na ambaye pia ni naibu mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA, Pernille Kardel amesema kuwa ulinzi wa wanawake katika vita, kuzuia unyanyasaji dhidi yao na pia kuwashirikisha katika utatuzi wa migogoro na kuzuia msimamo mkali ni muhimu kwa amani endelevu.

Bi Kardel ameyasema hayo katika sherehe ya siku ya kimataifa ya wazi iliyofanyika katika mkoa wa Nangarhar. Sherehe hiyo imehudhuriwa na karibu watu 40 ikiwa ni pamoja na Gavana wa Mkoa wa Laghman, Abdul Jabar Naeemi , Naibu Gavana wa Nangarhar, Muhamad Hanif Gardiwal, pamoja na wanaharakati wa haki za wanawake, wawakilishi wa mashirika ya kiraia kutoka mikoa ya mashariki ya Kunar, Laghman, Nuristan na Nangarhar huko Afghanistan.

Bi Kardel ameongeza kuwa wanawake ndio wanaoathirika zaidi na vikundi vyenye msimamo mkali vilivyo ikumba jamii huko mashariki mwa nchi. Siku hii maalum ya wazi ilizinduliwa mwaka 2010 kwa sababu ya maadhimisho ya miaka 10 ya azimio nambari l1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu wanawake na suala la amani na usalama.