Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya vifo DRC yaongezeka, Baraza la Usalama lapaza Sauti

Idadi ya vifo DRC yaongezeka, Baraza la Usalama lapaza Sauti

Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mapigano kati ya vikosi vya serikali na wafuasi wa vyama vya upinzani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imeongezeka na kufikia 32.

Mapigano hayo yalianza jumatatu asubuhi, na Jumanne iliripotiwa ghasia zilizosababisha ofisi za makao makuu ya vyama vitano vya upinzani kuchomwa moto.

Kufuatia ongezeko hilo la ghasia na maafa, wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameeleza wasiwasi mkubwa juu ya hali ya usalama nchini humo ambapo Rais wa baraza hilo kwa mwezi huu wa Septemba, Balozi Gerard van Bohemen wa New Zealand amesoma taarifa mbele ya waandishi wa habari.

(Sauti ya Balozi)

“Wakirejelea azimio namba 2277 la baraza, wajumbe wamesisitiza umuhimu wa uchaguzi wa rais ulio huru, wazi utakaofanyika kwa uhalali, kwa wakati na uwe shirikishi. Wamesema mchakato uzingatie katiba ya nchi kwa ajili ya utulivu, maendeleo na uimarishaji wa demokrasia DRC.”