Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Laos yaanzisha lengo lake la 18, SDG kuondoa mabomu yaliyosalia ardhini

Laos yaanzisha lengo lake la 18, SDG kuondoa mabomu yaliyosalia ardhini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambaye yuko ziarani huko Laos, hii leo ameisifu nchi hiyo kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa lengo lake la 18 ikiongezea yale ya maendeleo endelevu, SDGs.

Lengo hilo ni la kuondoa mabomu ya ardhini ambayo bado hayajalipuka, UXO yenye madhara makubwa kwa binadamu.

Ban ameipongeza Laos kwa hatua hiyo akisema inaonyesha nia ya pamoja ya kusaka amani, maendeleo endelevu yanayoweka watu kuwa kipaumbele na kuheshimu haki za binadamu.

Zaidi ya miongo mitatu tangu kumalizika kwa vita vya pili vya Indochina vikijulkana pia kama vita vya Vietnam ambapo mabomu ambayo hayakulipuka yanaendelea kuua na kulemaza watu wa Laos kila uchao.

Katika miaka 20 iliyopita, kupitia msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo  (UNDP) Laos imeweza kuondoa mabomu hayo kutoka eneo la kilometa za mraba 300 mraba na sasa ni ardhi inayotumika kwa matumizi salama.