Skip to main content

Takribani watoto milioni 50 duniani wang’olewa makwao- UNICEF

Takribani watoto milioni 50 duniani wang’olewa makwao- UNICEF

Ulimwenguni kote, takribani watoto milioni 50 wamekimbia makazi yao, zaidi ya nusu ya idadi hiyo ikiwa ni kutokana na mizozo na mapigano kwenye nchi zao.

Hiyo ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, katika ripoti yake iliyotolewa leo ikiangazia ongezeko la janga la wakimbizi na wahamiaji watoto.

Ripoti hiyo imesema idadi iliyosalia wanakimbia makwao kusaka maisha bora na usalama lakini wale wakiwa njiani wanakumbwa na majanga zaidi ikiwemo kuzama baharini, njaa, utapiamlo na hata usafirishaji haramu.

Mkurugenzi mkuu wa UNICEF Anthony Lake anahoji ni mustkhabali gani ambao unaandaliwa iwapo watoto hao hawana uhakika wa maisha yao hivyo wamependekeza mambo sita ikiwemo kulinda watoto wahamiaji na wakimbizi wanaosafiri wenyewe dhidi ya ghasia na ukatili, kuondoa uwekaji korokoroni watoto wanaosaka hifadhi na kuweka mbinu mbadala.

image
Mtoto Jannat Raslan na kaka yake ambao ni wakimbizi kutoka Syria wakibembea katika makazi yao ya ukimbizini huko Ujerumani. (Picha:© UNICEF/UN026295/Gilbertson VII Photo)
Halikadhalika familia kuwekwa pamoja, watoto hao kupatiwa fursa ya kujifunza, kushughulikia masuala yanayoshinikiza watoto kukimbia na kuendeleza hatua za kukabiliana na chuki dhidi ya wageni na ubaguzi.

UNICEF inasema Uturuki ndio yenye idadi kubwa zaidi ya watoto wakimbizi na wahamiaji kulingana na idadi ya watu wake sanjari na Lebanon ambako mtu mmoja kati ya watano ni mkimbizi.