Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali za Maziwa Makuu zaazimia kutokomeza vikundi hasimu Mashariki mwa DRC

Serikali za Maziwa Makuu zaazimia kutokomeza vikundi hasimu Mashariki mwa DRC

Mawaziri wa Ulinzi kutoka ukanda wa Maziwa Makuu, wamekutana jijini Nairobi leo Julai 20, 2016 kutathmini ufanisi na changamoto katika juhudi za kumaliza vikundi hasimu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na katika ukanda mzima.

Aidha, mkutano huo umelenga kuboresha na kuimarisha mkakati wa pamoja wa kukomesha biashara haramu inayofanywa na vikundi hivyo katika ukanda wa Maziwa Makuu.

Katika miaka michache iliyopita, serikali katika ukanda wa Maziwa Makuu na jamii ya kimataifa zimekuwa zikijikita katika kusaidia juhudi za serikali ya DRC kupambana na vikosi hasimu ndani ya mipaka yake.

Taarifa ya pamoja ya Umoja wa Mataifa, Kamati ya Kimataifa ya ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Muungano wa Afika (AU), imesema kutokomeza vikundi vyenye silaha mashariki mwa DRC ni muhimu katika kuleta utulivu DRC na katika ukanda mzima.