Skip to main content

Mkurugenzi wa WFP kushuhudia athari za El Niño Malawi

Mkurugenzi wa WFP kushuhudia athari za El Niño Malawi

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP Bi Ertharin Cousin, anazuru Malawi wiki hii kushuhudia athari za ukame uliosababishwa na El Niño.

Ukame huo ni mbaya zaidi kuwahi kuikumba Malawi katika historia. WFP inasema ombi la haraka la msaada wa dharura linahitajika ili kutoa chakula kwa watu milioni 6.5 walioathirika.

Msaada huo wa kibinadamu utakuwa ni mkubwa kabisa kuwahi kutolewa katika historia ya taifa hilo. Akiwa nchini humo kuanzia leo , Bi Cousini atajadili tatizo kubwa la njaa linalolikumba eneo zima la kusini mwa Afrika , tatizo ambalo linatarajiwa kuongezeka katika miezi ijayo kutokana na mavuno hafifu mwezi wa Aprili.

Fedha za ufadhili zilizopo sasa hazitoshi na Bi Cousin atajadili pia hatua za haraka kuepusha janga kubwa zaidi kutokana na ukosefu wa fedha.

Watu milioni 18 hivi sasa katika nzi zilizoathirika vibaya za Lesotho, Madagascar, Msumbiji, Swaziland, Zambia, Zimbabwe, na Malawi wanahitaji msaada wa haraka wa chjakula Kusini mwa Afrika, idadi ambayo huenda ikaongezeka hadi milioni 33 kutokama na uatabiri wa shirika la maendeleo kwa nchi za Kusini mwa Afrika SADC. Mataifa hayo karibu yote ikiwemo Botswana yametangaza hali ya dharura , huku Msumbiji ikitangaza hali ya hatari kutokana na ukame unaondelea kukumba nchi hizo.

WFP hadi sasa imepata robo tu ya dola milioni 549 zinazohitajika kwa operesheni za msaada wa dharura hadi 2017.