Siku chache zijazo ni muhimu katika kusaka amani Syria- De Mistura

Siku chache zijazo ni muhimu katika kusaka amani Syria- De Mistura

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura, amesema kuwa kuna shughuli nyingi za kidiplomasia zinazoendelea katika kusaka amani nchini Syria, na kwamba siku chache zijazo zitakuwa muhimu katika kuonyesha msimamo wa wenyekiti wenza wa mchakato huo wa kisiasa.

Bwana de Mistura amesema hayo jijini Geneva Uswisi akikutana na wanahabari, ambapo amesema wenyekiti hao wenza wakikubaliana kuhusu suala fulani, inasaidia kusongesha mbele mchakato wa kisiasa na hata ule wa kibinadamu.

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa sintofahamu inayolizingira suala la al-Nusra ndiyo moja ya changamoto kuu zinazokabili uendelevu wa usitishaji uhasama.

Amesema iwapo utapatikana muafaka kuhusu jinsi ya kupunguza au kukomesha urushaji wa mabomu ya angani kiholela na kuwa na utaratibu wa mpito wa kisiasa, basi awamu ya tatu ya mazungumzo baina ya Wasyria itakuwa siyo tu fanisi, bali huenda ikawa ndio mwanzo wa matokeo madhubuti katika masuala hayo, lakini pia katika mpito wa kisiasa.