Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP imelaani uporaji kwenye ghala lake la chakula Juba

WFP imelaani uporaji kwenye ghala lake la chakula Juba

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP limesikitishwa na kukasirishwa na uporaji kuliofanyika katika ghala lake kuu mjini Juba.

Licha ya changamoto hiyo kubwa WFP inasema wafanyakazi wake tayari wanagawa msaada wa chakula kwa watu waliotawanywa na mapigano kwenye mji huo mkuu wa Sudan Kusini.

Kwa ombi la WFP walinzi wa amani wa mpango wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini UNMISS wamefanya tathmini kwenye ghala hilo Jumatano na kutoa taarifa ya uporaji mkubwa wa chakula , ingawa wafanyakazi wa WFP bado hawajaweza kufika kwenye ghala hilo kuthibitrisha kiwango cha uporaji huo wa chakula.

Kabla ya kuzuka upya vita wiki iliyopita ghala hilo lilikuwa na zaidi ya tani 4,500 za chakula , ambacho kinatosheleza kutoa msaada wa kuokoa maisha na lishe kwa takribani watu 220,000 kwa muda wa mwezi mmoja Pia ghala hilo lilikuwa linahifadhi malori, jenereta na vifaa vingine visivyo chakula.

WFP imelaani vikali wizi huo wa chakula ambacho ni kwa ajili ya masikini na wasiojiweza Sudan Kusini. Na kuongeza kuwa pigo hilo litaathiri uwezo wao wa kuwasaidia maelfu kwa maelfu ya watu waliokimbia nyumba zao kwa sababu ya machafuko.