Uongozi Sudan Kusini umeshindwa na kuangusha watu wake:Ban
Mapigano mapya Sudan Kusini yanashtua, kusikitisha na kudhalilsha, na ni pigo lingine katika mchakato wa amani nchini humo.
Hayo ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon, amesema machafuko hayo yanaongeza madhila kwa mamilioni ya watu na kukebehi jitihada za kuleta amani ya kudumu.
Mamia ya watu wameuawa na kuna hofu inayoongezeka kwamba watu wengi zaidi watapoteza maisha katika machafuko hayo.

(SAUTI YA BAN KI-MOON)
“Kwa mara nyingine, viongozi wa Sudan Kusini wamewaangusha watu wao, ni nadra kwa nchi kufuja ahadi namna hii na kwa haraka sana. Ni uongozi wa aina gani ambao unaamua kutumia silaha za mauaji na utambulisho wa kisiasa tena na tena?ni uongozi ulioshindwa.”


Hivyo amelitaka Baraza la Usalama na wanachama wote wa Umoja wa Mataifa kusimama kidete wakati huu na kulinda haki za binadamu za watu wa Sudan Kusini. Katika maswali na majibu Ban amesema anatumai miongoni mwa hatua Baraza la Usalama iliiwekee sudan Kusini vikwazo vikiwemo vya silaha.