Liberia yashika hatamu za ulinzi kutoka UNMIL
Hatimaye serikali ya Liberia imechukua majukumu kamili ya ulinzi kutoka ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMIL ikiwa ni kwa mujibu wa azimio namba 2239 la mwaka 2015 la baraza la usalama.
Kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha hatua hiyo akipongeza azma ya wananchi wa Liberia ya kusaka amani ya kudumu baada ya kumalizika kwa mzozo wa wenyewe kwa wenyewe uliosababisha kupelekwa kwa UNMIL mwaka 2003.
Ban katika taarifa kupitia kwa msemaji wake ameeleza kuwa kuendelea kuimarishwa kwa usalama na utulivu nchini Liberia kumewezesha Umoja wa Mataifa kuingia hatua ya mwisho ya ulinzi wa amani nchini humo.
Ametambua dhima kutoka kwa wadau hususan jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, Muungano wa Afrika na jumuiya ya Mano katika kuwezesha kupatikana kwa amani ya kudumu Liberia sanjari na kudhibiti mlipuko wa Ebola uliotikisa nchi hiyo.
Ban ametoa wito kwa wadau hao kuendelea kusaidia Liberia kuimarisha amani.