Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukiukaji wa haki za binadamu na kutozingatia sheria kunaendelea Libya:UM

Ukiukaji wa haki za binadamu na kutozingatia sheria kunaendelea Libya:UM

Kutoheshimu maisha ya binadamu na kutozingatia utawala wa sheria ni hali inayoendelea Libya imesema ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa ofisi hiyo Ijumaa iliyopita watu 12 waliohusiana na utawala wa hayati Muammar Gaddafi , ambao waliachiliwa kutoka jela ya Al-Baraka siku moja kabla kwa mujibu wa amri ya mahakama mjini Tripoli, wamekutwa wamekufa.

Wanafamilia waliotambua maiti hao wamesema wahanga hao walikula kipigo kizito, kuteswa na pia kupigwa risasi mara kadhaa.

Wengine walikuwa na makovu ya kuungua na maiti zao zilikuwa zimefungwa mikono na miguu.

Ofisi ya haki za binadamu inasema utesaji na mashambulizi dhidi ya raia ni uhalifu chini ya sheria za kimataifa.

Na imeitaka mamlaka ya Libya kufanya haraka uchunguzi wa kina ili kuwafikisha kwenye mkono wa sheria wahusika.