Skip to main content

Ulemavu wa ngozi si kikwazo chochote kwangu- Keisha

Ulemavu wa ngozi si kikwazo chochote kwangu- Keisha

Jina Keisha ni maarufu si tu nchini Tanzania ambako mwanamuziki huyo wa kike anaendesha shughuli zake za muziki, bali pia sasa limetambuliwa na wataalamu huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa. Kisa? ni jinsi mwanamuziki huyo alivyoruka viunzi vya ubaguzi na hata kutovitambua na kuendelea na maisha yake. Wataalamu hao huru katika taarifa yao kuelekea siku ya kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu haki za watu wenye ulemavu wangozi wametambua watu mbali mbali mashuhuri ambao sasa ni mfano katika jamii kuwa ulemavu wa ngozi si sababu ya watu hao kunyimwa haki zao za msingi kama binadamu wengine. Wataalamu hao huru wametaja watu wengine kuwa ni pamoja na Naibu Waziri nchini Tanzania Dkt. Abdallah Possi, mwanamuziki nyota kutoka Mali Salif Keita , Yellowman wa Jamaica na Moses Swaray wa Liberia. Assumpta Massoi wa Idhaa hii amezungumza na Keisha ambaye jina lake halisi ni Hadija Shabaan na kuanza kwa kumuuliza iwapo anakumbana na changamoto zozote..