Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA yapazia sauti mahitaji ya wakimbizi wa ndani Sirte, Libya

OCHA yapazia sauti mahitaji ya wakimbizi wa ndani Sirte, Libya

Tathmini mpya ya mahitaji ya kibinadamu ya wakimbizi wa ndani huko magharibi mwa mji wa Sirte nchini Libya, imeonyesha kuwa nusu ya wakimbizi hao wanakabiliwa na hatari ya kujeruhiwa au kuuawa kwa kutumia silaha ndogondogo.

Kwa mujibu wa Shirika la Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), ni chini ya asilimia 25 tu ya familia za wakimbizi ndizo zinazoweza kujikimu kimaisha katika eneo hilo, na kwamba zinategemea usaidizi kutoka kwa jamaa, marafiki, na mashirika ya kitaifa na kimataifa.

Aidha, wakimbizi hao wa ndani wanakabiliwa na changamoto za makazi, na huduma za maji safi na kujisafi.

OCHA imesema, mpango wa jitihada za kibinadamu nchini Libya kwa mwaka 2016 unahitaji dola milioni 166 ili kusaidia watu milioni 1.3 walioathiriwa na mzozo nchini humo, ingawa umepokea asilimia 26 tu ya ufadhili.