Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tume huru ya uchunguzi ya UM kutathimini tena haki za binadamu Burundi

Tume huru ya uchunguzi ya UM kutathimini tena haki za binadamu Burundi

Wataalam huru watatu wa Umoja wa Mataifa wanaochunguza haki za binadamu Burundi (UNIIB) wataenda tena nchini humo kwa ziara ya pili kuanzia Juni 13 hadi 17.

Ziara hii ya pili itakuwa ni fursa ya kutathmini maendeleo ya hali ya haki za binadamu ambayo yamepatikana tangu ziara yao ya kwanza mwezi Machi mwaka huu na kuendelea na majadiliano na wadau wote katika mzozo unaoendelea wa Burundi.

Kwa mujibu wa Christof Heyns, mwenyekiti wa tume hiyo huru ya uchunguzi, wakiwa Burundi watakutana na viongozi wa serikali na wadau wengine wa kisiasa, wajumbe wa asasi za kiraia, wahanga wa ukiukwaji wa haki za binadamu, mashirika ya misaada ya kibinadamu yakiwemo ya Umoja wa mataifa na washirika wa kikanda nchini humo.

Tume hiyo huru ilipeleka wajumbe wa haki za binadamu Mei mwaka huu kusaidia kukusanya taarifa za ukiukaji wa haki za binadamu uliotekelezwa mwaka 2015 nchini Burundi.

Wajumbe wameshaanza kazi yao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, lakini pia wataenda Rwanda, Uganda na Tanzania katika wiki chache zijazo kuwahoji wakimbizi wa Burundi na kukusanya taarifa.