Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kauli za Rais Jammeh dhidi ya Mandika ni za kuchukiza- Dieng

Kauli za Rais Jammeh dhidi ya Mandika ni za kuchukiza- Dieng

Mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu udhibiti wa mauaji ya kimbari, Adama Dieng ameshutumu hotuba ya kuchukiza iliyotolewa na Rais Yahya Jammeh wa Gambia katika mkutano wa kisiasa mapema mwezi huu.

Katika hotuba hiyo Rais Jammeh ameripotiwa kutishia kutokomeza kabila la Mandinka akitaja kuwa ni maadui na wageni na kwamba atawaua mmoja baada ya mwingine hadi pale nzi asiweze kuwaona.

Bwana Dieng amesema kauli hiyo kutoka kwa rais ni ya kushtua kwani inajenga unyanyapaa na vitisho dhidi ya watu wa jamii ya Mandinka.

Amesema kauli kama hizo kutoka kwa kiongozi wa nchi zinadhihirisha kutokuwajibika na ni za hatari kupindukia na zinaweza kuchochea mgawanyiko miongoni mwa wananchi pamoja na ghasia.

Mshauri huyo amesema kauli kama hizo ni kiashiria cha onyo akisema kuwa ilishuhudiwa Bosnia na Rwanda na hivi karibuni Mashariki ya Kati jinsi uchochezi wa ghasia unaweza kusababisha mauaji ya halaiki.

Amemkumbusha Rais Jammeh kuwa uchochezi wowote wa chuki kwa misingi ya dini, kabila ambao unaweza kusababisha ubaguzi ni kinyume na sheria za haki za binadamu za kimataifa halikadhalika sheria za kitaifa.

Amemtaka ahakikishe kuwa haki za watu wote nchini Gambia zinalindwa bila kujali makabila au imani zao za dini.