Eritrea imetekeleza uhalifu dhidi ya binadamu- Ripoti

Eritrea imetekeleza uhalifu dhidi ya binadamu- Ripoti

Vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu vimetekelezwa nchini Eritrea katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, imesema tume ya Umoja wa Mataifa iliyoundwa kuchunguza haki za binadamu nchini humo.Taarifa kamili na John Kibego.

(Taarifa ya Kibego)

Ripoti imetolewa leo ambapo mwenyekiti wa tume hiyo Mike Smith amesema watu kugeuzwa wategemezi, kufungwa, kutoweka, kuteswa, kubakwa na kuuawa ni miongoni mwa uhalifu huo katika nchi ambayo imebainika hakuna taasisi za kidemokrasia kama vile bunge na mahakama huru.

Akizungumza na wanahabari mjini Geneva, Uswisi wakati akiwasilisha ripoti hiyo, Bwana Smith amesema vitendo hivyo vinafanyika kwa kificho sana ikiwemo watu kuingizwa jeshi la kujenga taifa kwa kipindi kisichojulikana na la kusikitisha..

(Sauti ya Mike)

"Tume imebaini kuwa uhalifu uliobainika, umetekelezwa kimsingi moja kwa moja au kwa njia nyingine na maafisa wa serikali au chama tawala, makamanda wa jeshi na maafisa wa usalama wa taifa. Tume imebaini watuhumiwa na itawasilsiha majina ya watu hao kwa kamishna wa haki za binadamu ili kusaidia hatua za baadaye za uwajibikaji.”

Ripoti ya leo ni ya pili inafuatia ya awali iliyotolewa mwaka mmoja uliopita ikitaja uhalifu nchini Eritrea, na hivyo tume ya sasa ilitakiwa ibaini iwapo uhalifu unaoendelea ni dhidi ya binadamu au la.