Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za haraka zinahitajika kukabili kusambaa kwa homa ya manjano Angola

Hatua za haraka zinahitajika kukabili kusambaa kwa homa ya manjano Angola

Hofu ya kuendelea kusambaa kwa homa ya manjano nchini Angola na kwingineko imelifanya shirikisho la msalaba mwekundu na mwezi mwekundu (IFRC) kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kukabili hali hiyo.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa IFRC kanda ya Afrika Dr Fatoumata Nafo-Traoré, upungufu wa chanjo, uchafu, mfumo wa kufuatilia kusambaa kwa maradhi na watu kuvuka mpka kila uchao kunaweza kufanya mlipuko huo wa kitaifa kuwa janga kubwa endapo hatua za haraka za kijamii hazitochukuliwa.

Kati ya nchi tano jirani zilizoripoti kuingiziwa ugonjwa huko kutoka Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Congo Brazzaville sasa zinamaambukizi katika sehemu mbalimbali za nchi zao.

Mbali ya juhudi zinazofanywa na shirika la afya duniani WHO, shirika la kuhudumia watoto UNICEF na wadau wengine IFRC inapeleka timu Angola kufanya tathimini na mahitaji na mapengo yaliyopo ili kusaidia kudhibiti maambukizi zaidi.