Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

O’Brien atoa wito usaidizi uongezwe kwa Wasyria wenye uhitaji

O’Brien atoa wito usaidizi uongezwe kwa Wasyria wenye uhitaji

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kibinadamu, ambaye pia ni mratibu wa misaada ya dharura (OCHA), Stephen O’Brien, ametoa wito usaidizi zaidi utolewe kwa Wasyria wenye uhitaji ndani ya Syria na katika ukanda mzima wa Mashariki ya Kati.

Bwana O’Brien ameutoa wito huo mwishoni mwa ziara yake kule Hatay, kusini mwa Uturuki, ambako amekutana na wakimbizi, wakiwemo watoto katika hifadhi ya watoto yatima ya Reyhanlý, waliosimulia jinsi familia nyingi zilivyokimbia kutafuta usalama.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya OCHA, hali ya kibinadamu ya mamilioni ya Wasyria katika ukanda mzima ni tete, watu milioni 6.5 wakiwa wamefurushwa makwao ndani ya nchi, na wengine milioni tano wakiwa wamekimbilia nchi jirani.

Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa, raia wa Syria milioni 13.5 katika ukanda mzima wa Mashariki ya Kati wanahitaji aina moja au nyingine ya usaidizi wa kibinadamu na ulinzi.