Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanaokimbia Fallujah wahitaji msaada- OCHA

Wanaokimbia Fallujah wahitaji msaada- OCHA

Wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya kibinadamu yaliyoko nchini Iraq wamesema raia walioko Fallujah, wako katika hatari kubwa kutokana na kwamba wamenasa katikati ya eneo la mapigano.

Mratibu wa masuala ya kibinadamu na mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibanadamu, OCHA, nchini Iraq, Lise Grande amesema wanapokea ripoti za kutisha kuhusu raia walionasa kwenye mapigano wakihaha kukimbilia maeneo yenye usalama.

Amekumbusha kuwa pande zote kwenye mzozo zinapaswa kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu na kufanya kila wawezalo kulinda raia na kuhakikisha wanapata misaada ya kuokoa maisha yao.

Tangu tarehe 22 mwezi huu, raia 800 wamekimbilia mahali salama ikiripotiwa kuwa baadhi ya familia zimelazimika kutembelea kwa saa nyingi na katika mazingira magumu kusaka usalama.

Bi. Grande amewahakikishia wakazi wa Fallujah kuwa watoa misaada ya kibinadamu wanafanya kila wawezalo kuwapatia mahitaji muhimu na kwamba tayari wamesambaza chakula, maji na malazi kwa wale wanaowasili maeneo salama.