Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshauri wa UM Benomar ziarani Burundi

Mshauri wa UM Benomar ziarani Burundi

Mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi Jamal Benomar anasafiri leo kwenda mji mkuu Bujumbura kufuatia mazungumzo yaliyofanyika awali wiki hii mjini Arusha Tanzania kuhusu mchakato wa kisiasa nchini Burundi.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa habari mjini New York Marekani, na kuongeza kwamba Bwana Benomar amejadiliana na wadau mbalimbali kwenye mazungumzo hayo na kusisitiza umuhimu wa mchakato jumuishi ili kupata mustakhabali wa amani kwa Burundi.

Kupitia akaunti yake ya Twitter, bwana Benomar amesema ,anatumai mazungumzo ya Arusha yatakuwa hatua ya kwanza katika kufanikisha huo mchakato.

Ameongeza kuwa hiyo ni changamoto kubwa na yeye pamoja na timu yake wako tayari kusaidia juhudi za mhamasishaji wa mazungumzo bwana Benjamin Mkapa.

Pia amepongeza bwana Mkapa kwa jitihada zake akiunga mkono uamuzi wake wa kukutana na wadau wa Burundi waliokataa kuhudhuria mazungumzo ya Arusha.