Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Macharia Kamau awa mjumbe maalum wa Ban kuhusu El Nino na tabianchi

Macharia Kamau awa mjumbe maalum wa Ban kuhusu El Nino na tabianchi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amewateua Balozi Macharia Kamau wa Kenya na Bi. Mary Robinson wa Ireland kuwa wajumbe wake maalum kuhusu masuala ya El Niño na mabadiliko ya tabianchi.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema uteuzi huu umekuja wakati wa dharura kubwa ambapo dunia imeshuhudia ukame na mafuriko yanayohusiana na El Nino hasa Afrika Mashariki, Kusin mwa Afrika, Amerika ya Kati na Pasifiki.

Kwa mantiki hiyo Ban amenukuliwa akisema Balozi Kamau na Bi. Robinson watatoa uongozi unaotakiwa kukabili changamoto hizo pamoja na kutoa tahadhari inapobidi.

Kwa sasa Balozi Kamau ni mwakilishi wa kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa ilhali Bi. Robinson ambaye aliwaku huwa Rais wa Ireland na kamishna mkuu wa haki za binadamu, anaongoza taasisi ya Mary Robinson inayoangazia haki na tabianchi.