Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wazidi kuhusishwa na mashambulizi ya kujitoa muhanga: OCHA

Watoto wazidi kuhusishwa na mashambulizi ya kujitoa muhanga: OCHA

Idadi ya watoto wanaotumikishwa na kundi la ugaidi la Boko Haram kwa ajili ya mashambulizi ya kujitoa muhanga imeongezeka mara kumi kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, sasa mshambuliaji mmoja kati ya watano wanaojitoa muhanga ni mtoto.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA, huku mkuu wa ofisi hiyo Stephen O’Brien akiwa amewasili leo mjini Nyamey, nchini Niger, kwa ajili ya ziara ya siku nne kwenye ukanda wa Ziwa Chad ulioathirika na mashambulizi ya Boko Haram.

Mwaka 2015, watoto 44 wamehusishwa na mashambulizi ya kujilipua, ikilinganishwa na wanne tu mwaka 2014.

OCHA imeongeza kwamba raia wanazidi kulengwa na mashambulizi ya kundi hilo, na hali ya kibinadamu kuzidi kuzoroto, ikieleza kwamba watoto 700,000 wameathirika na utapiamlo kaskazini mashariki mwa Nigeria pekee.