Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia zinazoendelea Syria zinaweza kuzusha zahma mpya kwenye maeneo yanayozingirwa:UM

Ghasia zinazoendelea Syria zinaweza kuzusha zahma mpya kwenye maeneo yanayozingirwa:UM

Nchini Syria wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wanaendelea kukabiliwa na changamoto wanapojaribu kuwasaidia raia wanaohitaji kwa udi na uvumba misaada ya haraka umesema leo Umoja wa mataifa.

Misafara ya misaada imepewa ruhusa ya kuwafikia karibu nusu tu ya watu 905,000 wanaohitaji msaada.

Jan Egeland, anayeongoza juhudi za Umoja wa Mataifa Geneva kwa ajili ya msaada kwa Syria amesema vikosi vya serikali vinawajibika kwa kiasi kikubwa. Akizungumza na waandishi wa habari amesema kazi ya kupeleka misaada itaendelea ingawa ni maeneo mawili tu kati ya 18 yanayozingirwa ndiyo yaliyoweza kupata msaada mwezi huu.

Ameongeza kuwa Aleppo Kaskazini mwa Syria ni moja ya maeneo hayo na lingine ni mji wa Moadamyia Kusini Magharibi mwa Damascus.

(SAUTI YA EGELAND)

“Moadamyia linaweza kuwa eneo la kutisha endapo hatutaruhusiwa kuingiza msaada, hakuna dhamana katika vita hivi vya kutisha na vya machungu kwa lolote inaonekana hasa inapokuja kwa raia.”

Jan Egeland anailaumu serikali kwa matatizo mengi ya kupata fursa lakini pia makundi ya watu wenye silaha.