Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yazindua mwongozo wa walimu kuhusu kuzuia itikadi kali katili

UNESCO yazindua mwongozo wa walimu kuhusu kuzuia itikadi kali katili

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), limezindua mwongozo mpya kwa walimu kuhusu kuzuia itikadi kali katili, ambao utawaelekeza katika kujadili suala hilo darasani.

Mwongozo huo umeandaliwa chini ya mkakati wa UNESCO unaohamasisha kuhusu uraia wa ulimwengu, na kwa kuitikia ombi la nchi wanachama la usaidizi katika kuimarisha sekta zao za elimu zinapokabiliana na itikadi kali katili.

Mwongozo huo unatarajiwa kuwasaidia walimu kuweka mazingira ya darasani yaliyo jumuishi na yanayotoa fursa kwa mazungumzo ya kuheshimiana, mijadala iliyo wazi, na fikra dadisi.

Halikadhalika, mwongozo huo unapendekeza rasilmali za kuongeza uelewa wa suala la itikadi kali katili na kutoa majibu kwa maswali yanayoulizwa mara kwa mara.