Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zambia inaweza kuwa bingwa wa kulinda haki za walemavu Afrika- UM

Zambia inaweza kuwa bingwa wa kulinda haki za walemavu Afrika- UM

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu, Catalina Devandas, amesema kuwa kuna fursa nzuri ya kutimiza haki za watu wenye ulemavu nchini Zambia, na kutoa wito kwa serikali ya nchi hiyo itekeleze kikamilifu baadhi ya sera na mikakati yake mizuri.

Mtaalam huyo amesema iwapo serikali ya Zambia itaweka kipaumbele utekelezaji wa sera na mkakati wa kisheria kuhusu ulemavu, basi inaweza kuwa bingwa katika masuala ya ulemavu kanda ya Afrika.

Mtaalam huyo wa Umoja wa Mataifa amemulika mikakati mingi iliyozinduliwa na mamlaka za Zambia ili kuboresha sera ya ulinzi wa haki za watu wenye ulemavu, ikiwemo kufanya utafiti kuhusu ulemavu nchini, pamoja na juhudi zilizofanywa katika kuufanya mkakati wa ulinzi wa kijamii kujumuisha watu wenye ulemavu.

Kwa mantiki hiyo, Bi Devandas ameihimiza serikali ya Zambia iendelee kufanya maendeleo katika kuwezesha haki ya watu wenye ulemavu kwenda wanakotaka, haki ya kupata elimu, afya, pamoja na kupata ajira, kwa kutekeleza sheria kuhusu watu wenye ulemavu na sera husika.