Skip to main content

Leo ni siku ya kimataifa ya mama dunia

Leo ni siku ya kimataifa ya mama dunia

Siku ya kimataifa ya mama dunia ni fursa muhimu ya kutanabaisha uhusiano tegemezi uliopo baina ya watu na viumbe mbalimbali ambavyo vinashirikiana dunia hii.

Hayo ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon katika ujumbe maalumu wa siku hii na kusema maadhimisho ya mwaka huu yanaleta matumaini ya mustakhbali wa watu wote.

Maadhimisho ya mwaka huu yanakwenda sanjari na tukio la kihistoria la utiaji saini mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, ambapo wawakilishi kutoka mataifa zaidi ya 170 wamekusanyika New York kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kudhibitisha ahadi zao.

Ban amesema historia hii inakwenda sambamba na utekelezaji wa malengo ya amendeleo endelevu ya ajenda ya mwaka 2030, ambayo inauwezo wa kubadili dunia.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “miti kwa ajili ya dunia”. Na mtandao wa siku ya mama dunia unapanga kupanda miti bilioni 7.8 katika miaka mitano ijayo.