Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila nchi iwe na baraza la watoto: Gordon Brown

Kila nchi iwe na baraza la watoto: Gordon Brown

Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu elimu Gordon Brown amesema bado jitihada zinahitajika ili kupaza sauti za watoto duniani kote na kuhakikisha haki zao zinaheshimiwa.

Bwana Brown amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa waandishi wa habari wakati ambapo ripoti mpya kuhusu haki za watoto inazinduliwa mbele ya Kamisheni ya Raia wa Kimataifa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Ameeleza kwamba Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu lililopitishwa mwaka 1948 halikuangazia suala la watoto ipasavyo.

Bwana Brown amemulika mapendekezo yaliyotolewa na ripoti hiyo yakiwemo kuunda mahakama ya kimataifa ya watoto ili kuchunguza masuala yanayowagusa kama vile utumikishwaji wa watoto au ndoa za utotoni.

Aidha amesema Umoja wa Mataifa unapaswa kuunda baraza la watoto ambalo lingeweza kukutana kila mwaka, na vilevile kila nchi inapaswa kuwa na bunge la watoto na kuliwekea bajeti ya kutosha.

Halikadhalika amependekeza:

(Sauti ya Bwana Brown)

“Ni lazima kuimarisha elimu kuhusu haki za binadamu na elimu kwa uraia, ili vijana wajitambue kama raia wa kimataifa. Elimu bora ya uraia inapaswa kuzingatia maadili yetu sote pamoja na kupambana na wale wanaosema kwamba kuishi pamoja na watu wenye dini au kabila tofauti haiwezekani.”