Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado misaada inahitajika katika maeneo yanayozingirwa Syria-De Mistura

Bado misaada inahitajika katika maeneo yanayozingirwa Syria-De Mistura

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa mataifa kwa ajili ya Syria amesema amehuzunishwa na kutokuwepo kwa hatua kubwa za kuwafuikishia misaada kwa watu wanaoihitaji nchini Syria.

Staffan de Mistura amesema tangu kuanza kwa mwaka huu watu 450,000 wamepokea msaada wa kibinadamu katika maeneo yanayozingirwa ambayo ni magumu kuyafikia pamoja na maeneo mengine muhimu .

Hata hivyo akizungumza mjini Geneva leo Alhamisi baada ya mkutano wa kikosi kazi cha kimataifa kwa ajili ya misaada ya kibinadamu Bwana de Mistura ameonyesha kuhuzunishwa kwake kwamba hakuna misafara mingine kuwafikia walengwa hali inayotia wasiwasi.

(SAUTI YA DE MISTURA)

"Siwezi kukataa kwamba kila mmoja kwenye mkutano amekatishwa tamaa na wengi kuhuzunishwa na kutokuwepo na misafara mipya inayofika kwenye maeneo ambayo mnajua yamekuwa yakifahamika kama yamezingirwa”

Na katika juhudi za kubadili hali hiyo, de Mistura ametangaza kwamba kikosi kazi hicho cha kimataifa kimejadili kuongeza shinikizo hasa katika ngazi ya juu bila kutoa maelezo zaidi. Pia amesema miaka mitano tangu kuanza kwa vita hivyo  kumekuwepo na watu zaidi ya 250,000 waliouwawa na huduma za kitabibu zinahitajika haraka nchini Syria.