Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi yakaribisha azimio la UM la kutuma vikosi vya polisi

Burundi yakaribisha azimio la UM la kutuma vikosi vya polisi

Serikali ya  Burundi imekaribisha  azimio la hivi karibuni la Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa la kutuma  vikosi vya polisi nchini humo kama sehemu ya jitihada za kumaliza mgogoro wa kisiasa  uliodumu karibu mwaka mmoja.  Kutoka Bujumbura, Ramadhan Kibuga anaarifu.

(Taarifa ya Kibuga)

Kwenye taarifa hiyo ya serikali ya Burundi iliosomwa na msemaji wake Philippe Nzobonariba, mamlaka za Burundi wamekaribisha vyema azimio la Umoja wa Mataifa 22 79 kama sehemu ya juhudi za kumaliza mgogoro wa hapa nchini.

"Serikali ya Burundi inapongeza juhudi zinazofafanywa na jumuiya ya kimataifa na hasa Umoja wa Mataifa unavyojighulisha na Bdi kusaidi kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayoikabili wakati huu . Ni kwa mantiki hiyo, serikali ya Burundi ilipokea vema azimio la 2279 lilopitishwa hivi karibuni na Baraza la la usalama Umoja wa mataifa tarehe mosi Aprili."

Aidha serikali imeridhia pia Kuletwa hapa nchini kwa vikosi vya Polisi, lakini msemajii wa serikali amebainisha msimamo wa serikali kuwa watakubali idadi ndogo mno ya polisi hao.

"Serikali ya Burundi inakubali ujio wa idadi ndogo tu ya askari polisi ambao wanaokadiriwa 20 hivi, tena wasio kuwa na silaha ambao wanaweza kuja kuimarisha na kunoa vikosi vya usalama katika hali ya kuimarisha haki za binaadamu nchini pamoja na kuendeleza uheshimishwaji wa sheria kwa ujumla. Serikali ya bdi inajiandaa kufanya mashauriano na Umoja wa Mataifa kuona jinsi wataalamu hao wa polisi wanavoweza kuja hapa Burundi."

Serikali ya Burundi imelipongeza pia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuzingatia kila mara uhuru na enzi vya Burundi kwenye maazimio yake na kuwa na yakini kuwa usalama wa nchi hii na raia wake kwanza ni shughuli ya serikali mbele ya watu wote.

Aidha kwenye taarifa hiyo ,serikali imekariri tena azma yake ya kuweka mbele mazungumzo ili kupatia ufumbuzi matatizo ya Burundi . Msemaji wa serikali amesema Tume ya Mazungumzo hapa nchini CNDI imejiandaa kushirikiana na wapatanishi wa ukanda ili kuwafikia warundi walioko nje nao waweze kutoka mchango wao.

Hata hivo serikali ya Burundi kwenye taarifa hiyo kwa mara nyingine imebainisha msimamo wake kwamba haiko tayari kuketi pamoja kwenye meza ya mazungumzo na wale ambao imewataja kuwa wamekuwa wanachochea vurugu hapa Burundi ikijenga hoja ya msimamo wake kuwa hata azimio la Umoja wa Mataifa la 22 48 la mwaka jana linaagiza kuwepo na mazungumzo na wadau wenye kuweka mbele amani.

Haya yanaarifiwa wakati mazungumzo kati ya serikali na upinzani yamekwama tangu yalipozinduliwa mwezi Disemba mwaka jana chini ya mpatanishi Rais Yoweri Museveni.