Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP na UNICEF zatoa wito wa dharura kwa usaidizi Mauritania

WFP na UNICEF zatoa wito wa dharura kwa usaidizi Mauritania

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa yameonya leo kuwa uhaba wa ufadhili unatishia uwezo wao kuendelea kutoa usaidizi muhimu kwa familia zilizo hatarini zaidi nchini Mauritania, kwa pamoja yakiomba ufadhili wa dola milioni 23 za Kimarekani kuweza kukidhi mahitaji.

Mashirika hayo ni lile la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ambalo linaomba ufadhili wa dola milioni 21, na lile la kuwahudumia watoto (UNICEF), ambalo linaomba dola milioni mbili za ziada.

Uhaba wa ufadhili tayari umeilazimu WFP kusitisha ugawaji wa mlo shuleni tangu mwezi Disemba, na hivyo kuwaacha watoto 150,000 kutoka familia maskini bila uhakika wa kupata angaa mlo mmoja kwa siku.

UNICEF imesema hali ya lishe nchini Mauritania ilizorota wakati wa msimu wa mwambo, na hivyo kuongeza idadi ya watoto walioathiriwa na utapiamlo, likionya kuwa bila usaidizi, idadi hiyo huenda ikapanda hata zaidi.

Mashirika hayo hushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa kutoa misaada kwa zaidi ya watu 380,000 wasio na uhakika wa kuwa na chakula, pamoja na zaidi ya watoto 130,000 chini ya umri wa miaka mitano, na akina mama na wajawazito 57,000 ambao tayari wanataabika au wamo katika hatari ya utapiamlo. Mashirika hayo pia huwasaidia wakimbizi 50,000 kutoka Mali.