Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malawi yafanyia jaribio matumzi ya droni katika kupima VVU

Malawi yafanyia jaribio matumzi ya droni katika kupima VVU

Serikali ya Malawi na Shirika la Kuhudumia Watoto (UNICEF), zimeanza kufanyia jaribio matumizi ya ndege zisizokuwa na rubani au droni, ili kutafuta njia bora za kupunguza muda wa kusubiri katika upimaji wa watoto kubaini maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU).

Likifanikiwa, Jaribio hilo ambalo linatumia sampuli za kuiga, linaweza kupunguza muda wa kusubiri kwa kiwango kikubwa, na litajumuishwa katika mfumo wa afya ili kusaidia mbinu nyigine kama usafiri wa barabarani na ujumbe mfupi wa rununu.

Katika jaribio hilo la kwanza, wakazi walitizama kwa furaha wakati ndege isiyo na rubani ikiruka kwa ufanisi kwa mwendo wa kilomita 10, kutoka kituo cha afya cha jamii hadi maabara ya Hospitali Kuu ya Kamuzu.

Safari hizo za majaribio ambazo zinatathmini gharama na usalama wa matumizi ya ndege hizo, zitaendelea hadi Machi 18.

Ndege zisizo na rubani zimetumiwa awali katika kufuatilia na kufanya tathmini ya mahitaji wakati wa majanga, ingawa hii ni mara ya kwanza ndege hizo kutumiwa katika kuimarisha huduma za afya dhidi ya VVU barani Afrika.