Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto 1 kati ya 3 Syria wanachokijua ni vita miaka mitano baada ya kuzuika mgogoro:UNICEF

Mtoto 1 kati ya 3 Syria wanachokijua ni vita miaka mitano baada ya kuzuika mgogoro:UNICEF

Watoto takribani milioni 3.7 wa Syria , mmoja kati ya watu wamezaliwa tangu kuzuka kwa mgogoro ambao sasa umetinga mwaka wa tano, maisha yao yameghubikwa na ghasia, hofu na kutawanywa imesema ripoti ya shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. Grace Kaneiya na taarifa kamili.

(Taarifa ya Grace)

Takwimu hizi zinajumuisha watoto zaidi ya 151,000 waliozaliwa kama wakimbizi tangu mwaka 2011.  Kwa mujibu wa UNICEF Zaidi ya asilimia 80 ya watoto wa Syria hivi sasa wameathirika na vita ama ndani ya nchi au kama wakimbizi katika nchi jirani. Imeongeza kuwa machafuko yamekuwa mazowea majumbani, mashuleni, hospitali, kwenye vituo vya afya, kwenye maeneo ya kucheza watoto na hata kwenye maeneo ya kuabudu.

Ukiukwaji mkubwa na unyanyasaji dhidi ya watoto pia umetajwa na ripoti hiyo  ikiwemo mauaji na uingizaji wa watoto vitani kama anavyofafanua Hanaa Singer mwakilishi wa UNICEF Syria

(SAUTI YA HANAA SINGER)

"Mtoto yeyote chini ya miaka mitano hajui chochote kando ya uharibifu, kuzingirwa na uharibifu wa maeneo, sio tu kwamba imeathiri hali yao ya kiafya lakini pia imeathiri elimu, Syria ilikuwa miongoni mwa nchi zilizoongoza katika uandikishaji wa watoto shuleni Mashariki ya kati lakini sasa huduma ya elimu imedorora mno."

Ripoti imesema changamoto kubwa katika mgogoro huo ni kuhakikisha watoto wanasoma. Imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua muhimu kulinda kizazi cha watoto hao.