Bidhaa za kitamaduni zinachangia ukuaji wa uchumi- UNESCO

Bidhaa za kitamaduni zinachangia ukuaji wa uchumi- UNESCO

Ripoti mpya ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), imeonyesha jinsi bidhaa za kitamaduni zilivyo na mchango mkubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi, hususani katika kizazi hiki cha digitali. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kutoka Chuo cha Takwimu cha UNESCO (UIS), biashara katika bidhaa za kitamaduni mathalan vito vya dhahabu, sanaa, sanamu, filamu na muziki, iliongezeka maradufu kati ya mwaka 2004 na 2013, licha ya mdororo wa uchumi wa dunia na wanaotumia bidhaa za filamu na muziki kuhamia kwenye mitandao ya intaneti.

Ripoti hiyo, inamulika kwa kina uuzaji na uagizaji wa bidhaa na huduma za kitamaduni duniani, ikionyesha kwamba biashara hiyo ilifikia thamani ya dola bilioni 212 mwaka 2013.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa Uchina imeipiku Marekani na kuongoza katika uuzaji wa bidhaa za kitamaduni nje, ingawa Marekani bado inaongoza katika kuagiza bidhaa za kitamaduni kutoka nje.

Kwa ujumla, nchi zilizoendelea zinachangia kwa kiasi kidogo uzalishaji wa bidhaa za kitamaduni zinazouzwa nje, ingawa zinaongeza katika kuziagiza.